SHILOH INTERNATIONAL MINISTRIES TANZANIA

Monday, March 24, 2014

JUMAPILI
 23/MARCH/2014.
 SOMO:JUMAPILI
 23/MARCH/2014.
 SOMO:
 

JINSI YA KUJITENGA NA UKOO WAKO ULETAO LAANA.
Na.Nabii Frank Julius Kilawah.

Kuna vitu ambavyo vinaendelea katika maisha uliyonayo,na wakati mwingine unapata shida kujitoa katika tatizo linalokusumbua kwa sababu ya LAANA ya ukoo wako.
Kwanza inabidi muelewe maana halisi ya neno LAANA ;
LAANA ni  hali ya kusogezwa chini kutoka chini au kutokufanikiwa kwa kiwango ulichokusudiwa au  kutokuuona wakati wako mpya au kutokubadilisha majira katika umri wako unaokuja na kwa lugha nyingine waweza kusema ni  kutokustawi au kutokuendelea.
Mtu mwenye laana siku zote hasongi mbele,bali laana humvuta mtu huyo chini ili aende chini
Kwa kuwa katika kila Ukoo kuna pande mbili,upande wa Baba na upande wa Mama,mtoto anapozaliwa anaunganika na laana za pande zote mbili,laana zinazotoka upande wa Baba na laana zinazotoka upande wa Mama.
Leo ninataka kukubadilisha ili uweze kubaki  na jina la ukoo,na kuziondoa chembe chembe zote za laana ya ukoo wako,unaweza kujiuliza LAANA hii inabaki vipi katika maisha yako, wakati unaenda mbele za mungu mara kwa mara kwa ajili ya TOBA.
Neno TOBA maana yake ni ubadilike unavyofikiri,na ni kweli Toba inaweza kujibu,lakini ni baada ya kwenda kwanza kwenye ASILI yako na kuiondoa LAANA ya ukoo wako.
Ezekiel 16:1 -3 Neno la Bwana likanijia tena, kusema,Mwanadamu,uujulishe Yerusalemu machukizo yake,useme,Bwana MUNGU auambia Yerusalemu hivi;Asili yako na kuzaliwa kwako kwatoka katika nchi ya Mkanaani;Mwamori alikuwa Baba yako,na Mama yako  alikuwa Mhiti.
Andiko hili linatuonyesha, kumbe kuna ASILI ya mtu,na katika maisha ya kawaida, ukizungumzia  Asili yako ina maamisha chimbuko la ukoo wako lilipoanzia,sasa kuna laana ambazo zimeanzia katika chimbuko la ukoo wako,ili uweze kupiga hatua kwenda mbele ni lazima ujitenge kwanza na laana hizo za ukoo wako.
Tunaona  ni namna gani  ASILI  yako inavyoweza kumzuia Mungu kuingilia kati matatizo uliyonayo,ili Mungu aingilie kati,mruhusu kwanza  aingie katika Asili ya Ukoo wenu.
YEREMIA 1:4-5 Neno la Bwana lilinijia,kusema,kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua,na kabla hujatoka tumboni ,nalikutakasa;nimekuweka kuwa Nabii wa kimataifa.
Andiko hili linamaanisha kwamba  kabla Mungu hajakupitishia  Kitovu  kutoka katika kitovu unachokijua alikujua,akakutakasa maana hakutaka ASILI yenu iambatane na wewe,na aliposema nimekuweka kuwa Nabii wa kimataifa inamaana hakuna siri itakayojificha kwako,unakuwa na taarifa ya kinachotokea kabla hakijatokea
Hujawahi kujiuliza kwa nini baadhi ya koo mtoto anapozaliwa wanadai Kitovu,nywele za kwanza,na wengine hudai hadi kondo la nyuma la mama anayejifungua, katika hali ya kawaida vitu hivyo ni uchafu,na baadhi ya familia mwanamke anapotaka kujifungua ni lazima aende akajifungulie kwao,umeshawahi kujiuliza ni kwa nini, ni kwa sababu wanatumia KITOVU chako  kukuunganisha na Asili ya ukoo wako,unapounganishwa,unaunganika  pamoja na LAANA za ukoo wako.
Kwa sababu hiyo ASILI yako inamzuia Mungu kuingilia kati matatizo uliyonayo mpaka utakapojitenga nayo kwa kumruhusu Mungu aingie kwanza katika ASILI ya ukoo wenu  na kuiondoa Laana.
Kuna mifumo mitatu ya Laana, ambayo ni laana ya afya,uhai na mafanikio, Hivyo ukitaka kutafuta chanzo cha kukwama kwako,rudi na uchunguze kati ya ASILI hizi mbili ya Baba yako na Mama yako na Mungu atasema nawe juu ya hilo kama ambavyo amesema nao katika kitabu cha Ezekieli ndivyo atakavyosema na wewe . 
Ukielewa ASILI yenu  utajua nini cha kufanya ,Mamajusi walielewa asili ya aliyezaliwa (Yesu Kristo) ndio maana hawakwenda mikono mitupu pia Nguvu ya Yesu kujifufua mwenyewe asili ya kitovu chake ni  mbinguni,lakini ili mauti yamfike asili ya kitovu chake  ni mwanadamu ambaye ndiye alimsulubisha Yesu na kumuua.
Asili uliyonayo haiwezi kukupatia kwanza unachokitaka,itakupatia usichokitaka mpaka pale utakapojitoa kwenye asili hiyo,kama ambavyo Mungu alipomwita Ibrahimu na kumwambia nataka nikuanzishie asili nyingine.
Ni watu wachache kabisa  katika kundi la watu waliookoka walioacha asili za kwao,wengi bado wanashiriki katika mambo ya asili za kwao kama matambiko,ujenzi wa makaburi na mengineyo hivyo kujiwekea kitanzi  na kushindwa kujitoa katika Asili zao.
Ili uweze kusonga mbele kiafya,katika Uhai na kimaendeleo ni lazima kwanza ujitenge na laana za ukoo wenu,Jitenge kwanza na asili za ukoo wenu uletao laana uweze kufunguliwa na kupokea muujiza wako.
   

JUMAMOSI
22/MARCH/2014.
SOMO
NGUVU YA UUMBAJI.
Na.Nabii Frank Julius Kilawah


Kuna vitu ambavyo watu wengi  wanaomcha Mungu hawavielewi, ndio maana hawavitumii  hivyo kutoa mwanya kwa waliopo upande wa pili wa Shetani kuvitumia.
Watu wengi waliookoka bado hawajatambua Nguvu ya Uumbaji,Yesu kristo ndiye mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote,  hivyo kuna nguvu kubwa sana ndani Uumbaji,ukiitambua nguvu hiyo utakuwa na uwezo mkubwa wa kumiliki mazingira unayoishi.
Wakolosai 1:15-16 Naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana ,mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote,kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa,vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi,vinavyoonekana na visivyoonekana;ikiwa ni vitu vya enzi ,au usultani,au enzi,au mamlaka;vitu vyote viliumbwa kwa njia yake,na kwa ajili yake.
Andiko hili linathibitishia kuwa  Yesu kristo ndiye mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote,neno hili likikaa katika fikra zako,hutaogopa chochote,hutakuwa na hofu juu ya magonjwa ya aina yeyote, maana hicho kijidudu kinachosababisha ugonjwa,kina mzaliwa wake wa kwanza ambaye ni Yesu Kristo.
Kwa hiyo tunatakiwa tuwe na uhakika kuwa juu ya magonjwa yote,kuna mzaliwa wake wa kwanza nayo humtii mzaliwa huyo ambaye ni Yesu Kristo.
Hii inakuthibitishia kiwango cha kumiliki na mamlaka uliyonayo ya kuamrisha  kila kiumbe kilichopo katika mazingira unayoishi kwa kulitumia jina la mzaliwa wa kwanza Yesu Kristo.
Kama unasumbuliwa na virusi vya ukimwi tambua Yesu ni mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote,,hata katika vijidudu vya ukimwi Yesu ni  mzaliwa wa kwanza wa vijidudu hivyo,kwa hiyo huna haja ya kuwa na hofu kwa maana kupitia jina la Yesu, vijidudu vya ukimwi vinafungasha virago na kuondoka katika damu yako na kuiacha ikiwa safi kabisa.
Marko 16:14-15 Baadaye akaonekana kwa wale kumi na mmoja walipokuwa wakila,akawakemea kwa kutokuamini kwao na ugumu wa mioyo yao,kwa kuwa hawakusadiki wale waliomwona alipofufuka katika wafu,akawaambia ,Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila KIUMBE.
Hapa Yesu akuwaambia mkaihubiri Injili kwa kila MTU,bali aliwaambia mkaihubiri Injili kwa kila KIUMBE kwa maana kila kiumbe kilichopo chini ya jua yeye ndiye mzaliwa wake wa kwanza.
Ukilijiua Neno hili vyema hutasumbiwa na mazingira unayoishi,chochote kinachotokea kisibadilishe akili yako, ukaacha kuamini unachokiamini,kwa maana nataka kukutambulisha kwa huyu anayeitwa mwanzo ili aanze na wewe katika ALFA na amalize na wewe katika OMEGA kwa kuwa ni yeye pekee ndiye mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote vilivyopo katika Mazingira unayoishi.

Thursday, March 20, 2014

TEMBEA KATIKA UWEPO WA ROHO MTAKATIFU



SOMO
TEMBEA KATIKA UWEPO WA ROHO MTAKATIFU.
Na.Nabii Frank Julius Kilawah
 16.03.2014

Kama mzaliwa wa pili baada ya Yesu Kristo, unatakiwa kuishi chini ya mwongozo wa Roho Mtakatifu katika kila jambo unalolifanya, wakati wote Roho Mtakatifu anapaswa kukuongoza juu ya nini cha kufanya na ukiwa naye ndani yako unakuwa na ujasiri wa kukabiliana na  jambo lolote linalokuja mbele yako. mfano kama ambavyo mlevi anayeongozwa na pombe anavyokuwa na ujasiri wa kupita katika msitu mnene huko akikutana na simba anakuwa na ujasiri wa  kumkabili.

Yohana 7:6 “Basi Yesu akawaambia, haujafika bado wakati wangu; ila wakati wenu siku zote upo”. Neno hili linatufundisha kuwa hatupaswi kufanya maamuzi yetu wenyewe pasipo kusubiri wakati wa Bwana,Mungu wetu. na wakati huo unatimilika pale Roho Mtakatifu anapokuongoza kufanya jambo hilo.

Wengi wanakwama katika mambo mengi kwa kuwa hufanya maamuzi kwa akili zao wenyewe bila ya kumsikiliza Roho Mtakatifu ,unapoongozwa kufanya jambo lolote na Roho Mtakatifu,Yesu Kristo anakusikia  lakini unapojiongoza mwenyewe katika mambo yako,mfano katika biashara,elimu, ndoa nk., hatokusikia bali utajisikia mwenyewe na watu waliokuzunguka.

Mzaliwa wa pili amepewa nafasi ya kuwa juu ya kila kiumbe chini ya jua na katika ulimwengu wa roho,usiache neema ya mzaliwa wa pili ukaukumbatia ulokole, Roho Mtakatifu hawezi hata siku moja kukupa nafasi ya kufurahia neema yake milele ikiwa haupo katika kusudi na mpango wa  Mungu  hivyo tambua kuwa  umezaliwa mara ya pili ili uwe chini ya uangalizi wa Roho Mtakatifu.

Mwanzo 25:34 na  Mwanzo 27:36 tunamuona  Yakobo ambaye ni mzaliwa wa pili anavyoipata haki ya mzaliwa wa kwanza katika uzao wa Isaka na kuzibeba Baraka zote alizostahili kuzipata Esau.
Shetani muda wote yupo kazini kuhakikisha haukai katika kusudi na mpango wa Mungu ,hivyo kama mzaliwa wa pili inakupasa ukae chini ya uangalizi wa Roho Mtakatifu.

 Wokovu ni kuishi katika mwongozo wa Roho Mtakatifu katika kila jambo ulifanyalo“Watu wote wanaoongozwa na Roho Mtakatifu hao ndio wana wa Mungu.”


Yohana 14:26

        "Lakini huyo msaidizi, huyo Roho Mtakatifu ambaye Baba atampeleka kwa Jina langu atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia"